Airtel kutumia internet ya Elon Musk Afrika
Sisti Herman
May 7, 2025
Share :
Airtel Afrika imeingia mkataba wa ushirikiano na SpaceX ili kutoa huduma za internet ya Starlink ya kasi ya juu kwa wateja wake barani Afrika. Lengo la ushirikiano huu ni kuimarisha upatikanaji wa internet katika maeneo ya mashambani na yasiyofikiwa na mitandao ya kawaida ya simu. Starlink tayari imepata leseni za kufanya kazi katika nchi tisa kati ya 14 ambazo Airtel Afrika inahudumu, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Kenya, Zambia, Malawi, Rwanda, Niger, Chad, Madagascar, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Leseni za nchi zilizosalia tano (Tanzania, Uganda, Gabon, Jamhuri ya Kongo, na Seychelles) ziko katika mchakato wa kupatikana.
Kupitia ushirikiano huu, Airtel Afrika itatumia teknolojia ya satelaiti za Starlink zinazozunguka kwenye obiti ya chini ya dunia (LEO) ili kuimarisha huduma zake za internet, hasa kwa Biashara, shule, na vituo vya afya katika maeneo ya vijijini. Aidha, Airtel itachunguza matumizi ya teknolojia ya Starlink kwa ajili ya "cellular backhaul" ili kupanua wigo wa huduma za simu za mkononi katika maeneo magumu ya ardhi. SpaceX itafaidika kwa kutumia miundombinu ya Airtel iliyopo ardhini, kama vile mitandao ya simu na vifaa vingine, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma zao.
Ushirikiano huu unalenga kushughulikia pengo la kidijitali barani Afrika kwa kuhakikisha kwamba watu binafsi, Biashara, na jamii katika maeneo ya mbali wanapata huduma za internet zinazotegemeka na za bei nafuu. Hata hivyo, changamoto za gharama za huduma za Starlink, ambazo zimeonekana kuwa za juu kwa watumiaji wa kipato cha chini, zinaweza kuathiri upatikanaji wa huduma hizi kwa baadhi ya wateja. Airtel Afrika inatarajiwa kutafuta njia za kupunguza gharama au kuunganisha huduma hizi kwa njia zinazowafikia wengi.
Chanzo; Techpoint Africa.