Aziz Ki kutamba na jezi nyekundu na nyeupe msimu ujao.
Joyce Shedrack
May 19, 2025
Share :
Kiungo wa klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Burkina Faso Stephane Azizi Ki anatarajia kujiunga na klabu ya Wydad Casablanca ya Nchini Morocco siku chache zijazo kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia ngazi ya klabu.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa nyota huyo amecheza mchezo wake wa mwisho akiwa na jezi ya Yanga siku ya leo na muda wowote ataondoka Nchini kuelekea Nchini Morocco.
Mjumbe wa kamati ya utendaji Yanga Alex Ngai amethibitisha juu ya taarifa zinazomuhusisha kiungo huyo kuondoka klabuni hapo kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
“Ni kweli inaweza ikawa leo ndiyo mechi yake ya mwisho anaelekea huko anakoelekea kwa sababu kuna michuano anaenda kucheza na wanamuhitaji haraka sana” Amesema Alex Ngai.
Aziz Ki ambaye alijiunga na Yanga msimu wa mwaka 2022/23 akitokea Asec Mimosas amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu yake mpya ya Wydad AC.
Nyota huyo mpaka sasa msimu huu amehusika kwenye jumla ya magoli 15 kwenye ligi kuu soka Tanzania bara akifunga magoli 9 na kutoa pasi 6 za magoli.