Barca na Inter hapatoshi leo UEFA
Sisti Herman
April 30, 2025
Share :
Ligi ya Mabingwa Ulaya inaendelea tena leo Aprili 30, 2025 kwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya pili baada ya ile ya jana iliyoishuhidia Washika Mitutu, Arsenal wakishindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kukubali kichapo cha 1-0 dhidi ya Paris Saint-German katika dimba la Emirates.
Leo Barcelona ambao ni Mabingwa wa klabu Bingwa Ulaya mwaka 2015 watakuwa wenyeji wa Mabingwa wa mwaka 2010, Inter Milan wakati ambapo miamba hiyo ya Uhispania ina kumbukumbu nzuri ya kutwaa kombe la Copa del Rey kwa kuwafunga 3-2 mahasimu wao Real Madrid kwenye fainali.
Inter Milan inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi tatu mfululizo kwenye Serie A huku ikiangazia kutinga fainali yake ya pili kwa kipindi cha misimu mitatu baada ya kupoteza 1-0 mbele ya Manchester City kwenye fainali msimu wa 2022/23 huku Barcelona ikitafuta fainali yake ya kwanza tangu msimu wa 2014/15 ilipotwaa kombe hilo kufuatia ushindi wa 3-1 dhidi ya Juventus kwenye fainali.
Timu hizo zimekutana mara 12 kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Barcelona imeshinda mara 6, sare 4 huku Inter Milan ikishinda mara 2 huku Barcelona ikiwa na kumbukumbu ya kuondoshwa kwenye hatua hii msimu wa 2009/10 kufuatia ushindi wa jumla wa 3-2.
Barcelona iliyokuwa ikinolewa na Pep Guardiola ilipokea kipigo cha 3-1 kwenye mchezo wa kwanza kabla ya kushinda 1-0 kwenye marudiano huku Inter iliyokuwa ikinolewa na Jose Mourinho ikitinga fainali na kutwaa kombe hilo kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Bayern Munich kwenye fainali ya mwaka 2010.
Mchezo huo utachezwa kuanzia saa 4 usiku kwenye dimba la Olímpic Lluís Companys.