Benjamin Mkapa (BMH) yapandikiza figo mgonjwa wa 50
Eric Buyanza
January 2, 2025
Share :
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya mkoani Dodoma imefanikiwa kumpandikiza figo kwa mafanikio mgonjwa wa 50 tangu kuanza kutoa huduma hiyo miaka sita sasa huku Sh bilioni 1.6 zikiokolewa, hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi.
“Takribani miaka sita iliyopita Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikuwa kituo cha pili hapa nchini kutoa huduma ya bobezi ya upandikizaji figo, huku akisema kwa sasa gharama ya matibabu kwa mgonjwa mmoja ni wastani wa Sh milioni 34 ikilinganishwa na wastani wa Sh milioni 64 kama mgonjwa huyo angetibiwa nje ya nchi India na Ulaya.
Wagonjwa hao 50 waliopandikizwa hapa Benjamin Mkapa, asilimia 95 wanaishi na kuendelea na majukumu yao,” alisema Profesa Makubi.
Alisema takribani asilimia 98 ya wagonjwa wanaopandikizwa figo wanaendelea kuishi na kufanya majukumu yao baada ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kupata huduma hiyo, huku wastani wa asilimia 86 wakiendelea kuwa hai baada ya miaka mitano tangu kupata huduma.
“Hii inaonesha ubora wa huduma hii hapa nchini kuwa ni mzuri kwa viwango vinavyofanana na maeneo mengine duniani kama Marekani, Ulaya na India,” alieleza.
Akizungumzia gharama “Hivyo kupandikiza figo wagonjwa hao 50 tangu Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanza kutoa huduma ya ubingwa bobezi wa upandikizaji figo, serikali imetumia takribani Shilingi bilioni 1.7 ikilinganishwa na takribani Shilingi bilioni 3.3 endapo wananchi hao wangetibiwa nje ya nchi, hivyo kuokoa takribani Shilingi bilioni 1.6,” alifafanua Profesa Makubi.