Bingwa wa zamani wa Ulaya na Olimpiki aendesha kliniki ya ngumi.
Joyce Shedrack
May 2, 2025
Share :
Bingwa wa zamani wa Ulaya na mshindi mara mbili wa medali za Olimpiki bondia Nouchka Fontijn kutoka Uholanzi, jana siku ya Mei Mosi ameendesha kliniki ya mchezo wa ngumi pamoja na kugawa vifaa katika Jiji la Dar es salaam.
Bi. Nouchka alieambatana na Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Mh. Lukelo Willilo na Mwenyekiti wa kamati ya wanawake na wachezaji wa BFT Bi. Asha Voniatis, aliendesha kliniki 2 za mchezo wa ngumi kwenye Klabu ya BBC iliyopo Manzese Tip Top, Jengo la CCM kata ya Manzese na badae kumalizia Manzese Darajani na mabondia chipukizi wakiongozwa na Mahad Bakari.
Kliniki hizo zilizokuwa na lengo kubwa kuwalenga mabondia chipukizi wa rika zote pamoja na wanawake, zilifanikiwa sana na kuongeza hamasa kwa wachezaji chipukizi pamoja na wanawake kujitoa zaidi kushiriki mchezo wa ngumi.
"Nimefarijika sana kujumuika na vijana na kuwafundisha mbinu mbalimbali za mchezo huu, pia nimefurahia kutimiza ndoto yangu ya kugawa vifaa katika Afrika, hasa hapa Tanzania" alisema Nouchka.
Nouchka amesafiri alfajiri ya leo kuelekea Mkoa wa Arusha na ataendesha Kliniki nyingine na kugawa vifaa huko kabla ya kuelekea kwenye safari yake ya utalii kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na vivutio vingine.
Nouchka, bondia mkubwa nchini Uholanzi aliyestaafu mwaka 2021 akicheza uzani wa middleweight 75kg, amefanikiwa kushinda medali mbili katika Olimpiki (Fedha - Rio 2016 na Shaba - Tokyo 2020), Ubingwa wa Dunia (Shaba - Jeju 2014, Fedha - Kazakhstan 2016 na Fedha - New Delhi 2018)
Pia ameshinda Ubingwa wa Ulaya (Dhahabu - Sofia 2018 na Fedha - Rotterdam 2011) na Ubingwa wa mashindano ya Ulaya (European games Baku 2015 - Dhahabu)
Fainali za Olimpiki Rio 2016 na Ubingwa wa Dunia Astana 2016 alizoshinda medali za Fedha, alipoteza dhidi ya Clarissa Shields kutoka Marekani na Bingwa wa sasa wa Dunia undisputed heavyweight wa WBC, WBA, IBF na WBO.