Ekari 157 za mashamba ya Bangi zateketezwa Kondoa
Sisti Herman
May 23, 2025
Share :
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kondoa pamoja na wananchi wa Kata ya Haubi, wamefanikisha operesheni maalum ya kutokomeza kilimo haramu cha bangi katika maeneo ya Hifadhi ya Milima ya Haubi, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa mamlaka, Daniel Kasokola, amesema operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Mei 14 hadi 19, imefanikisha uteketezaji wa ekari 157 za mashamba ya bangi yaliyokuwa katika vijiji vya Ntomoko, Kinyasi na Haubi.
Aidha, watuhumiwa saba wanashikiliwa kwa mahojiano huku pikipiki mbili zikikamatwa katika maeneo ya operesheni.
“Operesheni hii ni ya pili kufanyika mwaka huu katika wilaya ya Kondoa. Januari tulibaini na kuteketeza zaidi ya ekari 500 za bangi. Kupungua kwa mashamba haya hadi ekari 157 ni ushahidi kuwa wananchi wameanza kuelewa na kushiriki kikamilifu katika jitihada hizi. Tunawapongeza kwa ushirikiano huu,” amesema Kasokola.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatuma Nyangasa, amesisitiza kuwa serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana kwa karibu na DCEA katika kuhakikisha kilimo cha bangi kinatokomezwa kabisa na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa ili waachane na kilimo hicho haramu na badala yake wajikite katika uzalishaji wa mazao halali ya chakula na biashara kama vile tumbaku, ufuta na maharage.
“Tunawaomba wananchi waachane na kilimo haramu cha bangi. Serikali ipo tayari kuwaongoza katika kuelekea kilimo halali na chenye tija. Ushirikiano baina ya serikali na wananchi ndiyo silaha kubwa ya kuikomboa jamii yetu,” amesisitiza Nyangasa.