Fernandes amtaja kocha sahihi wa kuinoa United
Eric Buyanza
May 22, 2025
Share :
Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes amemtaja "kocha sahihi" wa kuifundisha klabu hiyo baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa UEFA Europa League.
Kumbuka kwamba Fernandes alishindwa kuiokoa Man United kutoka kwenye kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye fainali ya Ligi ya Europa usiku wa jana.
Bao pekee la Brennan Johnson kipindi cha kwanza liliipa Spurs ushindi dhidi ya Mashetani Wekundu mjini Bilbao.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Man United Ruben Amorim alitoa kauli akisema atakuwa tayari kuondoka Old Trafford ikiwa uongozi wa klabu hiyo utaamua kumtimua.
Hata hivyo, Bruno Fernandes anasema bado anaamini mreno mwenzake Ruben Amorim ndiye kocha sahihi wa kuinoa United.
Kiungo huyo wa kati wa Ureno anaunga mkono United kubakia na Amorim, licha ya matokeo mabaya ya timu tangu alipokabidhiwa mikoba kutoka kwa Erik ten Hag Novemba mwaka jana.
"Nadhani Ruben Amorim ndiye mtu sahihi," Fernandes aliviambia vyombo vya habari baada ya mchezo wa jana usiku.
“Najua ni vigumu kuelewa, lakini bado naamini ni kocha sahihi.
"Klabu iko katika hali ambayo ni rahisi kuwa na kocha mpya kwa sababu matokeo hayajapatikana. Lakini nadhani ni mtu sahihi," alisema.