Gattuso kocha mpya timu ya Taifa Italia
Sisti Herman
June 16, 2025
Share :
Gennaro Gattuso sasa ndiye kocha mpya wa timu ya taifa ya Italia. Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) limetangaza uteuzi wake rasmi jana Jumapili, wiki moja tu baada ya Luciano Spalletti kufutwa kazi kutokana na kipigo cha 3-0 kutoka kwa Norway kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia. Gattuso atatambulishwa rasmi kama kocha mpya wa Azzurri Alhamisi, kwenye hoteli ya Parco dei Principi, Rome.
Gattuso ni jina kubwa kwenye historia ya soka la Italia. Akiwa mchezaji, alichezea timu ya taifa mechi 73 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 2006. Amewahi pia kuiongoza Napoli kutwaa taji la Coppa Italia mwaka 2020. Safari yake ya ukufunzi ilianza mwaka 2013 kama kocha-mchezaji wa Sion nchini Uswisi, na tangu wakati huo ameongoza klabu tisa tofauti, ikiwemo AC Milan, Valencia ya Hispania na Marseille ya Ufaransa.
Kocha huyo mwenye miaka 47 anarejea kwenye ramani ya juu ya soka akiwa na kazi moja kubwa mbele yake: kuipeleka Italia kwenye Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico. Italia hawajacheza Kombe la Dunia tangu 2014, hali iliyowapa presha FIGC kuhakikisha wanarudi kwenye ramani. Gattuso anaanza kazi rasmi huku Italia wakiwa nafasi ya tatu kwenye kundi lao la kufuzu, wakijiandaa kuvaana na Estonia na Israel mwezi Septemba.
Awali, Claudio Ranieri alikuwa chaguo la kwanza la FIGC, lakini alikataa ofa hiyo akiamua kubaki kama mshauri mwandamizi ndani ya klabu ya Roma. Hii imefungua milango kwa Gattuso kurudi kwenye majukumu ya juu, safari yake ikianza tena akiwa na matumaini makubwa na presha ya kurudisha heshima ya Azzurri.