Hashim Mbaga adadavua timu za Tanzania kwenye CAF Rankings
Sisti Herman
September 23, 2024
Share :
Kutokana na mikanganyiko ya taarifa zinazochapishwa mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii kuhusu msimamo wa viwango vya vilabu barani Afrika (CAF Rankings), aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa idara ya Wanachama wa klabu ya Simba Hashim Mbaga ametoa tathmini ya kina kuhusiana na CAF Rankings kwa namna inayoeleweka zaidi.
Anaandika Hashim Mbaga
NAJUA WAJUA ILA NATAKA KUKUJUZA ZAIDI NA ZAIDI KUHUSU RANKING POINTS ZA CAF.
Na: Hashim Mbaga. 23/09/2024
HISTORIA FUPI
Mwaka 2016 CAF walifanya mabadiliko makubwa ya Kimfumo wa uendeshaji wa Mashindano yake yaweze kujitegemea na pia kujipima yenyewe bila kuchanganya Mashindano mengine ya vilabu kwa nchi wanachama na kuweka System (Mifumo) mipya ya Ranking kwa utaratibu wa Point ambazo zitakuwa zinatoa uwiano ndani ya Miaka mitano ya Ufanisi kwa Timu ndani ya Mashindano yake chini ya CAF Interclub.
Katika Mfumo mpya uliotangazwa na CAF ambao ulipaswa kuanza katika Msimu Mpya 2018 ikabadili mambo makubwa yafuatayo:
1. Kuanza kuacha kutaja mwaka 2018 na kuwa Msimu 2018-2019
2. Kuongeza Timu Toka 8 hadi 16 zinazoingia Group Stage
3. Ranking zitaanza kwa Miaka 5 toka mwaka uliopo kurudi nyuma kwa maana msimu wa 2018-2019 ulikusanya Point kuanzia 2015.
4. Ikitokea Nchi zinafungana itaangaliwa mafanikio mazuri ya karibuni
5. Matokeo ya msimu huu yatatumika katika hesabu za msimu ujao
6. Ranking Point za Champions league zitakuwa kubwa tofauti na Confederation Cup.
7. Kutakuwa na Level 2 za Utaratibu wa Kupata Point ambazo zitapelekea kuwa na Rank baada ya Level moja kwenda ingine kila Level (Hatua) imegawanyika katika Categories (Vitengo) Vitatu na vyote ni lazima vya kufuata.
Kutokana na Utaratibu huu Tanzania ikaweza kuingia Katika Nchi 12 Bora na kuweza kushirikisha Timu 4 kwa mara ya kwanza katika msimu wa 2019-2020, Tanzania ilipata nafasi hii ingawa walifungana Point na Nchi ya Ivory Coast ni kutokana na mafanikio ya Simba kwa Msimu uliopita kwa mara ya kwanza baada ya kuingia Robo Fainali ya CAF Champions league msimu wa kwanza 2018-2019 wakati timu ya Asec iliishia Group na kutolewa baada ya kuwa ya mwisho katika kundi lake.
TANZANIA NA TIMU ZAKE
Toka Kuanza Mfumo mpya wa Ranking 2018 hadi sasa msimu wa 2024-2025 ni jumla ya Misimu 8 ambako Tanzania imeweza kuingia katika Utaratibu katika misimu SABA kwa Timu 3 katika nafasi 11 Tofauti tofauti ndani ya CAF INTERCLUB, Namungo 1, Yanga 4 na Simba 6.
2018 - YANGA - Group Final Confederation Cup
2018-2019 SIMBA - Quarter Final Champions league
2020-2021 SIMBA - Quarter Final Champions league, NAMUNGO - Group Stage Confederation
2021-2022 SIMBA - Quarter Final Confederation Cup
2022-2023 YANGA - Final Confederation Cup, SIMBA - Quarter Final Champions league
2023-2024 YANGA - Quarter Final Champions league, SIMBA - Quarter Final Champions league
2024-2025 (Ndio Unaendelea sasa), YANGA - Group Stage Champions league , SIMBA - Group Stage Confederation Cup
MSIMU HUU WA 2024-2025 UNAOENDELEA
Ushiriki wa msimu huu 2024-2025 wa Timu Nne za Tanzania ni matokeo ya ukusanyaji Point ndani ya Miaka Mitano toka 2019-2020 hadi 2023-2024 na kuwepo katika RANKING BORA ambako katika kipindi hicho Tumeweza kama Tanzania kuingiza Timu TATU katika Misimu MINNE MFULULIZO iliyopelekea kuendelea kupata Uwakilishi na kwa msimu Unaofuata pia.
Safari nzuri sana ya Tanzania ilianza 2021-2022 iliweza kukusanya Jumla ya Point 30.5 ambazo zilipatikana Toka Yanga 0.5, Namungo 2 na Simba 28 na kuweza kuingiza Timu 4 msimu wa 2022-2023 ambao ulikuwa moja ya Msimu bora sana katika Historia ya Tanzania maana Ndio Msimu Timu ya Yanga iliweza kufika Fainali ya CAF Confederation Cup.
Katika Msimu huo wa 2022-2023 Tanzania iliweza kukusanya Point Mpya 35 ambako Yanga ilitoa 20 na Simba ilitoa 15 na kuchanganya na za nyuma zilizobaki Tanzania kufikisha jumla ya Point 56.5 zilizoitoa Tanzania katika Ranking ya nchi bora ya 11 na kupanda hadi nchi bora ya 6.
Kutokana na Tanzania kuwa katika RANK nzuri Nchi bora ya 6 msimu wa 2023-2024 iliweza kuendelea kupata Uwakilishi wa Timu 4 katika CAF Interclub na Msimu huo ilianza na Point 41 Toka 56.5 ilizokuwa nazo kabla na Kuingiza Timu 2 za Simba na Yanga katika Group Stage hadi Quarter Final ya CAF Champions league.
TANZANIA TUPO WAPI SASA
Uzalishaji wa Point za Msimu uliopita ni faida ya kuweza kupata RANK bora kwa msimu huu wa 2024-2025 ambao kihesabu hizi Point zinapatikana muda huu ila hesabu yake inahesabika msimu unaofuata sio sasahivi.
Kutokana na Hesabu ya Msimu uliopita 2023-2024 Timu za Simba na Yanga kila moja kuzalisha Point 15 na Kufanya Tanzania kuwa na Point mpya 30 ukiweka na za kabla 41 Tanzania inafikisha jumla ya Point 71 (Simba 39, Yanga 31, Namungo 1) ambazo zinapelekea Tanzania kuendelea kushika nafasi ya 6 kwa nchi yenye ubora kwa Vilabu na ukanda wa Cecafa kupata Vilabu Vitatu vilivyopo Juu ambazo ni Simba nafasi ya 7 (Point 39), Yanga Nafasi ya 13 (Point 31) na Al Hilal nafasi ya 16 (Point 25).
Tumeanza Msimu huu 2024-2025 Kwa Tanzania kuendelea kuwa nafasi ya 6 baada ya Timu za Yanga na Simba zote kuingia Group Stage na kuongeza Point kutoka 71 za nyuma zilizopungua na kubaki 52.5 na sasa Yanga iliyopo Champions league imeshaweka Point 5 na Simba iliyoko Confederation Cup imeweshaweka Point 2.5 na kufanya Jumla ya Point 60 kwa Tanzania.
Kwa upande wa Timu ya Yanga ambayo ilikuwa kabla na Point 31 zilipungua mpaka 24 na kuongeza mpya za sasa 5 inafanya kuwa na Point za kuanzia 29 zinazoitoa nafasi ya 13 mpaka kuwa nafasi ya 11.
Wakati Timu ya Simba ambayo ilikuwa kabla na Point 39 zilipungua mpaka 28 na kuongeza mpya za sasa 2.5 inafanya kuwa na Point za kuanzia 30.5 zinazoitoa nafasi ya 7 mpaka kuwa nafasi ya 8 nyuma ya TP Mazembe ingawa wamelingana Point sababu ni wingi wa ukusanyaji Point kwa msimu huu Mazembe 5 wakati Simba 2.5.
Katika Mashindano ya CAF INTERCLUB yanayoendelea sasa Timu zote Yanga na Simba zinasubiria Kupangwa kwa Ratiba ya Group Stage na ni matumaini kuwa zitaendelea kukusanya Point zaidi na kwenda Juu zaidi kama Tanzania.
PLAY FAIR, BE POSITIVE