Hivi ndivyo kura inavyopigwa kumchagua Papa
Eric Buyanza
April 29, 2025
Share :
Kufuatia kifo cha Papa Francis na mazishi yake kufanyika Jumamosi iliyopita, makadinali kutoka kote ulimwenguni watakusanyika kwenye kongamano litakaloanza Mei 7 kumchagua Papa wa 267.
Jumla ya makadinali 135 walio na umri wa chini ya miaka 80 ndio watakaostahili kushiriki katika kura hiyo ya siri ili kuamua ni nani atakuwa mkuu wa kanisa hilo lenye waumini Bilioni 1.4.
Wakati wa kongamano hilo, makadinali hawataruhusiwa kuwa na mawasiliano yoyote nje ya hapo na pia hawataruhusiwa kuwa na kifaa chochote cha mawasiliano kama vile simu.
Watakuwa wakiishi Casa Santa Marta - nyumba ya wageni ya ghorofa tano katika Jiji la Vatican - na kutembea kila siku hadi Kanisa la Sistine, ambapo mchakato wa upigaji kura hufanyika kwa siri.
Kila kardinali ataandika chaguo lake kwenye kura na kuiweka kwenye chupa kubwa la fedha na dhahabu ambapo mshindi anahitaji theluthi mbili ya wingi ili kuchaguliwa.
Wakati haya yote yanafanyika, Wakatoliki husubiri katika Uwanja wa St Peter's ulio karibu, wakitazama moshi uinuke kutoka kwenye bomba la Kanisa la Sistine, Moshi mweusi inamaanisha hakuna uamuzi, mweupe unaashiria Papa mpya amechaguliwa.