Huu hapa ujumbe mzito wa Binti wa Gaddafi akiwaonya wairan
Eric Buyanza
January 15, 2026
Share :

Aisha Gaddafi anayeishi uhamishoni nchini Oman, na ambaye alikuwa binti wa aliyekuwa Rais wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi ametuma ujumbe huu kwa watu wa Iran:
“Enyi watu thabiti na wapenda uhuru wa Iran!
Ninazungumza nanyi kutoka kwenye moyo uliojaa uharibifu, maumivu, na usaliti. Mimi ni sauti ya mwanamke ambaye alishuhudia uharibifu wa nchi yake, sio mikononi mwa maadui wa wazi, lakini baada ya kunaswa na tabasamu za udanganyifu za Magharibi na ahadi zake za uongo.
Ninawatahadharisha msikubali kuangukia kwenye maneno ya hadaa na nara za mabeberu wa Magharibi. Waliwahi kumwambia baba yangu, Kanali Gaddafi, ‘Ukiachana na mipango yako ya nyuklia na makombora, milango ya dunia itafunguka kwako.’
Baba yangu, kwa nia njema na uaminifu katika mazungumzo, alichagua njia ya makubaliano. Lakini mwishowe, tuliona jinsi mabomu ya NATO yalivyogeuza ardhi yetu kuwa kifusi. Libya ilizama katika damu, na watu wake sasa wamenaswa katika umaskini, uharibifu na wengine kukimbilia uhamishoni.
Dada na kaka zangu wa Iran, ujasiri wenu, adhma na uthabiti wenu mbele ya vikwazo, na vita vya kiuchumi ni uthibitisho wa heshima na uhuru wa kweli wa taifa lenu. Kuingia kwenye makubaliano na adui hakuleti chochote ila uharibifu, migawanyiko, na mateso. Kujadiliana na mbwa-mwitu hakutaokoa kondoo au kuleta amani ya kudumu; inaweka tu alama ya mlo unaofuata!
Historia imethibitisha kwamba wale waliosimama kidete kutoka Cuba hadi Venezuela, na Korea Kaskazini hadi Palestina - wanabaki hai katika mioyo ya mashujaa wa dunia na kuandika historia kwa heshima. Na wale waliojisalimisha wakawa majivu, majina yao yakasahauliwa.
Salamu kwa watu jasiri wa Iran!
Salamu kwa upinzani wa Iran!
Salamu kwa mshikamano wa kimataifa na watu wa Palestina!
Kwa upendo na huruma,
Aisha Gaddafi”.





