Juma Choki kucheza na Mtoto wa Bongani Saudia
Sisti Herman
May 20, 2025
Share :
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini na mshiriki pekee kutoka Tanzania, Juma Choki 'King of Ring' anatarajia kupanda ulingoni katika hatua 16 bora ya michuano ya kombe la Dunia la ngumi dhidi ya Bekizizwe Maitse 'Dr Sleep' wa Afrika Kusini ambaye ni mtoto wa kwanza wa bingwa wa zamani wa ABU, Bongani Mahlangu.
Mtanzania huyo ametinga hatua hiyo baada ya kumchapa Bryx Piala wa Ufilipino kwa pointi katika pambano la hatua ya 32 bora ya michuano hiyo iliofanyia Aprili 17, mwaka huu Ukumbi wa Global Theater Boulevad Riyadh City, Riyadh, Saudi Arabia.
Inatajwa mabondia hao watapanda ulingoni katika hatua hiyo katika pambano litakalopigwa Juni mwaka huu kwa tarehe itakayotajwa na Baraza la Ngumi Duniani 'WBC' ambao wanasimamia mashindano hayo.
Ikumbukwe, Bongani 'Profesa' amekuja kupigana nchini mara tatu ambapo mwaka 2021 alimchapa TKO, Mtanzania, Tony Rashid katika pambano la ubingwa wa ABU kabla ya Tony Rashid kulipiza kisasi cha kupigwa mwaka 2022 kwa kumchapa kwa pointi lakini mwaka 2023, Bongani alirejea tena katika pambano la kuwania ubingwa wa WBC Afrika dhidi ya 'Tanzania One, Fadhili Majiha na kupigwa kwa pointi.