Kenya yaunga mkono kauli ya Rais Samia
Sisti Herman
May 21, 2025
Share :
Akiongea na kituo cha Televisheni cha Citizen cha nchini Kenya mnamo Mei 20, 2025, Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri Kenya, Musalia Mudavadi ameiunga mkono kauli ya Rais Samia juu ya wanaharakati kutoka nje kuingilia mambo ya Tanzania.
“Sitaipinga [Kauli ya Rais Samia] kwa sababu nadhani kuna ukweli ndani yake. Tuangalie hoja kadhaa. Kiwango cha adabu, matusi tunayoyaona Kenya, pamoja na kuwa tuna uhuru wa maoni, kuna wakati kuna kuvuka mipaka,” Mudavadi anaeleza akijibu swali la mwandishi Yvonne Okwara.
Okwara alihoji kama serikali ya Kenya ina mpango wa kuchukua hatua za kulalamika kidiplomasia hasa juu ya hoja ya ‘watovu wa adabu’.
“Rais Samia anasema watu wanavuka mipaka [katika kutoa maoni] Kenya, huo ni ukweli,” Mudavadi anaeleza.”Mimi ni Mkenya pia, ukweli ni kuwa; namna tunavyofanya mambo na tunavyo ongea, kwa sababu kuna uhuru wa maoni, hakuna heshima,” Mudavadi alisisitiza.
Akiongea mnamo Mei 19, 2025, Rais Samia alionya juu ya wanaharakati kutoka nje wanaongilia mambo ya Tanzania, wengi wakihusisha kauli hiyo na wanaharakati aliofika Tanzania kufuatilia kesi ya Lissu wakitokea nchini Kenya.
“Tumeanza kuona mwenendo wa wanaharakati ndani ya region yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku,” alieleza Rais Samia.
“Tusitoe nafasi walishaharibu kwao, walishavuruga kwao nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu,” alifafanua zaidi.
“Kuna majaribio kadhaa, niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na nyinyi wasimamizi wa sera zetu nje kutokutoa nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kutovuka hapa kwetu,” aliagiza Rais Samia.