Mamlaka yakamata zaidi ya Kilo 1000 za Dawa za kulevya
Sisti Herman
November 12, 2024
Share :
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali Nchini kati ya October na November 2024, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya, mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya huku Watuhumiwa 58 wakikamatwa katika operesheni hizo.
Akiongea Jijini Dar es salaam leo November 12,2024, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya Mtuhumiwa “Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inavyosababisha madhara kiafya, vilevile hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka na mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa na magonjwa haya wamerogwa”
“Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi, dawa hizo ziliingizwa Nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika”
“Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya na kusababisha Wafanyabiashara na Watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya”