Marekani yashambulia na kuharibu boti 7 za kijeshi za Iran
Eric Buyanza
May 5, 2026
Share :

Rais wa Marekani Donald Trump amesema jeshi la nchi yake limeshambulia na kuziharibu boti saba ndogo za kijeshi za Iran katika Mlango bahari wa Hormuz, huku hali ya kijeshi katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji duniani ikiendelea kuwa tete.
Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la Marekani, mashambulizi hayo yalitekelezwa kwa kutumia helikopta. Hata hivyo, Iran bado haijathibitisha wala kukanusha madai hayo.
Operesheni hiyo ni sehemu ya mpango wa Marekani unaoitwa “Project Freedom”, ambao kwa mujibu wa Trump unalenga kusaidia meli zilizokwama na wafanyakazi wa baharini kuondoka salama katika Mlango wa Hormuz.
Hata hivyo, Iran inaendelea kusisitiza kuwa mlango huo bado umefungwa na imedai kufyatua risasi za onyo dhidi ya manowari za Marekani, madai ambayo Washington imeyakanusha vikali.
Operesheni hiyo ya kijeshi ya Marekani inahusisha meli za kivita na ndege zaidi ya 100 pamoja na wanajeshi takribani 15,000.
BBC





