Mke wa Rais wa Finland atembelea Makumbusho ya Taifa.
Joyce Shedrack
May 15, 2025
Share :
Mke wa Rais wa Finland Suzanne Innes-Stubb atembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania.
Ujio wa ziara hiyo umefanyika Mei 14/05/2025 Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kilichopo Posta, Dar es salaam.
Ziara hii ni utangulizi wa ziara ya hii leo tarehe 15/05/2025 ambapo Makumbusho ya Taifa inatarajia kumpokea Rais wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb, aliyewasili jijini Dar es Salaam, Tanzania kwa ziara rasmi ya siku tatu kuanzia Mei 14 hadi 16, 2025.
Akiwa kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Mke wa Rais wa Finland Bi. Suzanne Innes-Stubb alipokelewa kwa ngoma za asili kisha wenyeji wake Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Dkt. Noel Lwoga, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania walimkaribisha.
Akiongea baada ya kumpitisha maeneo mbalimbali na kujionea mikusanyo na historia ya Tanzania iliyohifadhiwa kituoni hapo Dkt. Lwoga amesema ni mafanikio makubwa ya Serikali ya awamu ya sita katika kuutangaza utalii lakini pia ni alama kwa Wizara ya mali asili na utalii katika kupanua wigo wa kutangaza vivutio vya utalii.
Naye Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii alisisitiza ziara hii inalenga kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Finland.