Mwalimu Erick mbaroni kwa kumjeruhi mwanafunzi kwa viboko
Eric Buyanza
May 19, 2025
Share :
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Ngilimba iliyopo kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, Erick Ombeni anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kumchapa viboko mwanafunzi wa darasa la saba Julius Paul (15) na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo liliotokea Mei 14 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi wakati mtihani wa moko ukiendelea katika shule hiyo, na alipigwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake ila aliumiza zaidi mgongoni.
Awali akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo Pauline Benedicto alisema, ilikuwa majira ya asubuhi ya tarehe 14 aliamka mapema kumuandalia mwanae chakula kwa sababu alikuwa kwenye mitihani na alipokuwa njiani kumpelekea alikuwa nae huku akiwa analia kwa uchungu.
Alisema, wakati akimhoji kulikoni kwanini analia ghafla alianguka chini na kumbeba mpaka nyumbani na kumhadithia kuwa ameshambuliwa kwa viboko na Mwalimu mkuu wake, ndipo alipochukua jukumu la kutoa taarifa katika uongozi wa serikali ya kijiji na mtendaji wa kata.
Pauline alisema, kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia mtoto wake waliandikiwa barua ya kumpeleka zahanati kupata huduma ya kwanza wakati wakimsubiria Mwalimu Mkuu kufika ofisi za kata kwa ajili ya kuyazungumza, lakini alishindwa kufika kwasababu alikuwa miongoni mwa wasimamizi wa mitihani.
Aidha alisema, walifika shuleni na Mwalimu mkuu alikiri kumpiga viboko mtoto wake kwa sababu ya kukosea mara kadhaa kwenye karatasi ya majibu wakati akifanya mtihani wa moko, na kutokana na hasira alizokuwa nazo alimpiga kupitiliza na kuomba msahamani juu ya tukio hilo.
Nae mwanafunzi huyo alisema, alikosea kuandika jina lake kwenye karatasi ya majibu wakati wakifanya mtihani wa moko ikachafuka, Mwalimu mkuu alimsimamisha mbele ya wanafunzi akimtaka kuandika ubaoni jina lake huku akimshambulia kwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake.
NIPASHE