Polisi wamkamata mmoja kushambuliwa kwa Padre Kitima
Sisti Herman
May 1, 2025
Share :
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Rauli Mahabi mkazi wa Kurasini, Dar es Salaam kwa tuhuma za kumjeruhiwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima ambaye taarifa za kushambuliwa kwa Padri huyo ilisambaa katika mitandao ya kijamii.
Taarifa ya Polisi imetolewa leo, Alhamisi Mei 1, 2025 na Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro imesema Jeshi la Polisi linamshikilia na kumhoji Mahabi, mkazi wa Kurasini kuhusiana na tukio la kushambuliwa kwa Padri Kitima lililotokea eneo la Kurasini, Temeke Jijini Dar es Salaam zilipo ofisi za TEC makao makuu.
“Anashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo. Uchunguzi wa kina unaendelea ili hatua kali na za haraka zichulikuliwe kwa wahusika,” ameeleza Muliro na kubainisha kuwa tukio hilo limetokea saa nne usiku wa kuamkia leo maeneo ya Baraza la Maaskofu Tanzania Kurasini, Temeke jijini Dar es Salaam.
“Padri huyo inadaiwa tangu saa tatu asubuhi (jana Jumatano) walikuwa na kikao na viongozi wa dini mbalimbali na baada ya kikao kuisha saa 1 jioni alikwenda kwenye kantini yao ambapo aliendelea kupata kinywaji hadi saa nne na robo alipokwenda maliwatoni pembeni ya kantini hiyo ndipo alidai kushambuliwa kichwani na kitu butu na watu wawili,” imeeleza taarifa hiyo ambayo imebainisha kuwa Padri Kitima amepelekwa Hospitali ya Aga Khan na anaendelea na matibabu.