Rais wa Namibia kufanya ziara Tanzania tarehe 20-21 Mei,2025.
Joyce Shedrack
May 19, 2025
Share :
Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt.Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kufanya Ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan.
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Namibia tarehe 21 Machi 2025 na inalenga kukuza ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika nyanja za biashara, uwekezaji na elimu,
Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kidugu na kidiplomasia, hivyo ziara hii itafungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowawezesha wananchi wa nchi zote mbili kunufaika kiuchumi
Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atapokelewa Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia ambapo viongozi hao wawili wanatarajia kuwa na mazungumzo ya uwili na kisha kuongoza mazungumzo rasmi baina ya nchi hizo mbili na baadae kuzungumza na waandishi wa habari.
Aidha, akiwa nchini Tanzania, Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atatembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama sehemu ya kuthamini mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi barani Afrika na pia kukuza ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni kati ya Namibia na Tanzania,.
Rais Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kuhitimisha ziara yake tarehe 21 Mei, 2025.