Rais wa zamani wa Nigeria afariki dunia
Sisti Herman
July 13, 2025
Share :
Rais wa zamani wa Nigeria, Muhammed Buhari, amefariki dunia leo Julai 13, 2025 wakati akipatiwa matibabu jijini London.
Buhari aliyeiongoza Nigeria mara mbili kama mkuu wa jeshi na rais amefariki akiwa na umri wa miaka 82, Shirika la Habari la AP limemnukuu katibu wake wa habari, Bashir Ahmad leo Jumapili.
Kupitia akaunti yake ya X (zamani Twitter) Ahmad ameandika: “INNA LILLAHI WA INNA ILAIHIR RAJI’UN. Familia ya rais huyo wa zamani imetangaza kufariki kwa Muhammadu Buhari, GCFR, mchana wa leo katika kliniki moja mjini London. Mwenyezi Mungu ampokee katika Aljannatul Firdaus, Amin.”
Ikumbukwe Buhari aliingia madarakani mwaka 2015, akisimamia kipindi kibaya zaidi cha uchumi nchini humo na kupambana na uasi.
Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Ikulu ya Nigeria, Buhari alizaliwa Desemba 17, 1942, huko Daura, Jimbo la Katsina, Nigeria. Aliiingia jeshini akiwa na umri mdogo mwaka 1961 na kupata mafunzo nchini Nigeria, Uingereza, India na Marekani.
Katika kipindi chote cha utumishi wake jeshini, alishikilia nyadhifa mbalimbali muhimu za kamandi na wafanyakazi, akipanda vyeo na kufikia Meja Jenerali.