RC Makonda awavutia Shirika la Nyumbu kufufua kiwanda cha General Tyre Arusha.
Joyce Shedrack
May 21, 2025
Share :
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, leo ameambatana na uongozi wa Shirika la Nyumbu katika ziara maalum ya kutathmini uwezekano wa kufufua Kiwanda cha General Tyre kilichopo jijini Arusha. Ziara hiyo inalenga kurejesha matumaini kwa wananchi wa Arusha kupitia mpango wa serikali wa kufufua viwanda vilivyokuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Makonda amesema kuwa serikali ina lengo la kuhuisha viwanda vilivyojenga historia ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo General Tyre, ambacho kilikuwa chanzo kikubwa cha ajira na pato la taifa na kuongeza kuwa kupitia Shirika la Nyumbu, kiwanda hicho kinaweza kurejea katika hali ya uzalishaji na kusaidia katika kupunguza tatizo la ajira nchini.
βTunataka kuona namna gani tunaweza kufufua kiwanda hiki, ambacho ni tumaini kwa wananchi wa Arusha. Lengo letu ni kuhakikisha viwanda kama General Tyre vinafufuliwa kwa ushirikiano wa karibu na taasisi za umma na binafsi,β amesema
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumbu, Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Yusuph Kisamba, ameeleza kuwa shirika hilo linaangalia uwezekano wa kuwekeza katika kiwanda hicho kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara na kuongeza kuwa tayari wameanza tathmini ya awali ya miundombinu na mahitaji muhimu kwa ajili ya uendelezaji wa kiwanda hicho.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumbu, Kanali Charles John Kalambo, amesema kuwa shirika lipo tayari kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama matairi, pasi aina ya Philips na vifaa vingine vya viwandani, kulingana na mahitaji ya soko la ndani na taasisi za serikali kama halmashauri na wizara mbalimbali.
Hata hivyo, Mhandisi Juma Kassim Kumbikila, ambaye ni mshauri wa kiufundi wa shirika hilo, amesema kuwa eneo la ekari 50.4 lililokuwa likitumika na General Tyre bado lipo katika hali nzuri na linaweza kutumika kwa upanuzi wa uzalishaji.
Mpango huu wa kufufua kiwanda cha General Tyre unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi mkoani Arusha, huku ukitoa fursa mpya za ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa viwanda nchini.