Trump, Elon Musk urafiki wao hali tete
Sisti Herman
June 8, 2025
Share :

Urafiki wa Rais wa Marekani Donald Trump na mfanyabiashara tajiri zaidi duniani Elon Musk sasa unaonekana kufikia ukingoni baada ya wawili hao kurushiana cheche za maneno makali na hata matusi kwenye mitandao ya kijamii.
Rais wa Marekani Donald Trump anasema ameshangazwa sana na kukatishwa tamaa na ukosoaji wa mshirika wa zamani Elon Musk kuhusu mswada wake mkuu wa bajeti.
"Mimi na Elon tulikuwa na uhusiano mzuri. Sijui kama tutakuwa marafiki tena," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House. Baada ya kauli hiyo, Musk alijibu kwa ujumbe mkali. Katika kujibu, Musk alimshutumu rais Trump kwa kumtaka kama mtu asiye na shukrani, na kuongeza: "Bila mimi, Trump asingeshinda uchaguzi".
Musk aliacha wadhifa wake katika Wizara ya Ufanisi wa Serikali hivi karibuni baada ya siku 129 kazini. Lakini katika siku chache tangu aondoke serikali, amekuwa akiukosoa mara kwa mara mswada wa bajeti ya Trump unaofanya kazi kupitia Bunge la Congress, akiuita wa " kuchukiza" na kuchapisha kwenye ukurasa wake wa X: "Aibu kwa wale walioupigia kura: unajua ulifanya vibaya."
Trump alichapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social : "Njia rahisi zaidi ya kuokoa pesa katika Bajeti yetu, Mabilioni na Mabilioni ya Dola, ni kusitisha Ruzuku na Mikataba ya Kiserikali ya Elon.
Siku zote nilishangaa kwamba Joe Biden hakufanya hivyo!" Katika ujumbe mwingine wa Twitter, ambapo Musk alinakili chapisho la Trump, anasema: "Kwa kuzingatia kauli ya Rais kuhusu kufutwa kwa kandarasi za serikali yangu, @SpaceX itaanza kuzima chombo chake cha anga cha Dragon mara moja".





