Waandishi 5 wa Al Jazeera wauawa na Israel Gaza
Eric Buyanza
August 11, 2025
Share :
Kituo cha habari cha Al Jazeera kimethibitisha kwamba waandishi wake watano wameuawa katika shambulio la anga la Israel lililotokea karibu na lango kuu la Hospitali ya Al-Shifa, mjini Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa ya kituo hicho, waandishi wa habari Anas al-Sharif na Mohammed Qreiqeh, pamoja na wapiga picha Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa, walikuwa ndani ya hema maalum la waandishi wa habari lililokuwa limewekwa katika hospitali hiyo, wakati walipolengwa moja kwa moja na shambulio hilo la Jumapili.
Al Jazeera imelitaja tukio hilo kama “ushambulizi mwingine wa wazi na wa kupangwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.”
Hata hivyo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilithibitisha baadaye kuwa lilimlenga Anas al-Sharif, likidai kupitia chapisho la Telegram kwamba alikuwa kiongozi wa kikosi cha wapiganaji wa Hamas.
IDF haikuwataja wala kueleza lolote kuhusu waandishi wengine waliouawa.
Jumla ya watu saba waliuawa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera.
Kituo hicho awali kilitangaza kuwa wafanyakazi wake wanne wamepoteza maisha, lakini baadaye kilisahihisha idadi hiyo na kuthibitisha kuwa ni watano.
BBC