Washinda mikeka baada ya kubashiri Papa mpya
Sisti Herman
May 12, 2025
Share :
Uchaguzi wa Papa Leo XIV (Robert Francis Prevost) haukuwa tu tukio la kidini lililofuatiliwa kwa makini na mamilioni ya waumini wa Kanisa Katoliki duniani, bali pia ulibadilika kuwa fursa ya kiuchumi kwa wacheza kamari waliobashiri matokeo yake.
Kabla ya Leo XIV, kutangazwa kurithi mikoba ya Papa Francis aliyefariki Aprili 21, 2025, katika makazi yake ya Mtakatifu Marta, Vatican, majina 12 ya makardinali waliokuwa wanapigiwa chapuo kuchaguliwa katika wadhifa huo ni Pietro Parolin (Italia), Luis Tagle (Ufilipino), Fridolin Ambongo Besungu (DRC), Matteo Zuppi (Italia) na Péter Erdő (Hungary).
Wengine ni, Anders Arborelius (Sweden), Pierbattista Pizzaballa (Italia), Juan José Omella (Hispania), Reinhard Marx (Ujerumani), Robert Sarah (Guinea) na Marc Ouellet wa Canada.
Katika hali ya kushangaza, Kardinali Prevost, ambaye hakutajwa sana katika mizunguko ya midahalo ya wachambuzi wa Vatican, ndiye aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo uliogubikwa na usiri mkubwa, na inaelezwa kuwa kuna wacheza kamari waliotumia tukio hilo la kihistoria kama fursa ya kupiga pesa.
Tovuti ya Jarida la Forbes imeripoti kuwa wacheza kamari mtandaoni walitumia zaidi ya Dola za Marekani milioni 40 (zaidi ya Sh107.9 bilioni) kubashiri juu ya atakayekuwa Papa mpya na mshindi mmoja alipata dola 52,000 (Sh140 milioni) kwa ubashiri wa hatari kuwa Prevost (Leo) atakuwa Papa.
Watu wengi walijaribu kubashiri ni nani angechaguliwa kuwa Papa mpya na hata kuweka pesa zao katika ubashiri huo. Wachache walitegemea kuwa angekuwa Mmarekani huyo kutoka Chicago, nchini Marekani.
Wacheza kamari waliwekeza kiasi hicho cha zaidi ya Sh107 bilioni katika mkutano wa hivi karibuni wa uchaguzi wa Papa, kupitia majukwaa mawili tu ya masoko ya utabiri: zaidi ya dola milioni 30 (zaidi ya Sh80 bilioni), kwenye Jukwaa la Polymarket, kulingana na tovuti yao, na zaidi ya dola milioni 10.6 (zaidi ya Sh28 bilioni) kwenye Kalshi, kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo.