Watu wananunua udongo wa Benki kama dawa ya kupata utajiri
Eric Buyanza
March 14, 2025
Share :
Huko nchini China watu wenye tamaa ya kupata utajiri haraka, wameweka imani kwenye mifuko ya "udongo wa benki" inayouzwa mtandaoni wakiamini inaweza kuwasaidia kuvuta utajiri.
Benki kadhaa za Uchina hivi karibuni zimekuwa zikiandamwa na watu wanaochota udongo nje ya maeneo yanayozunguka benki hizo na kwenda kuuza mtandaoni wakiwa wamefunga kwenye vifuko vidogo kwa dollar 120 (takriban laki 3 za Tanzania) huku wakisema ni dawa ya kuleta utajiri wa haraka.
Taarifa zinasema mahitaji ya bidhaa hiyo yanaongezeka kwa kasi kila kukicha nchini humo huku baadhi ya wauzaji wakiaminisha watu kuwa wengi wa wateja walionunua udongo huo wamepata mafanikio ya kifedha.
Tovuti moja ilidai kuwa aina nne za udongo wa benki inazouza zimekusanywa kutoka benki tano ambazo ni Benki Kuu ya China, Benki ya Viwanda na Biashara ya China, Benki ya Kilimo ya China, Benki ya Ujenzi ya China, na Benki ya Mawasiliano.
"Udongo huu unakusanywa kwa mikono kutoka benki tano na inaaminika unaleta utajiri, ingawa hatuwezi kuthibitisha hili kisayansi," alisema mwakilishi mmoja wa duka la mtandaoni aliyeongea na gazeti la South China Morning Post.