Yafahamu majina 6 ya utani aliyopewa Raila Odinga
Eric Buyanza
October 18, 2025
Share :
BABA
Baba, jina maarufu nchini Kenya ambalo Raila Odinga amehusishwa nalo kutokana na historia yake ndefu kwenye siasa.
Katika familia, 'Baba' ni mtu ambaye huchukuliwa kuwa kiongozi na hili ni jina ambalo limejitokeza kuonyesha ishara ya wafuasi wa Raila kwa jinsi wanavyompenda na kumuamini kama mzazi anayewaongoza vyema.
Na ndivyo wengi wanavyomchukulia Raila Odinga, kama baba yao hasa katika siasa aliyejinyima mengi kwa ajili ya demokrasia Kenya.
AGWAMBO
Agwambo ni jina la kabila la luo linalomaanisha mtu asiyetabirika au mwenye usiri mkubwa.
Wafuasi wake walimpa jina hilo kulingana na jinsi ambavyo alikuwa akiendesha siasa zake.
Kwa wanaomjua, watakumbumba vile ambavyo alikuwa akipinga serikali waziwazi, na sio kwamba anaishia hapo, bali wakati mwingine alifika hadi kiwango cha kuandaa maandamano na kushiriki nao kiasi cha hata kutembea na wafuasi wake barabarani wakipitisha ujumbe wao.
Mbinu hii ya ushirikiano wa karibu na wafuasi wake licha ya umri wake ulifanya waliompinga au wasiomuunga mkono wakiwa na wakati mgumu.
JAKOM
Jakom ni jina la luo linalomaanisha mtu ambaye ana wadhifa wa mwenyekiti, kiongozi wa kikundi fulani au mtu aliye na wadhifa wa juu na wenye mamlaka.
Jamii ya Waluo hutumia jina hilo kumtambua Raila kama kiongozi wa kabila hilo.
RAO
'RAO' ni ufupisho wa jina lake Raila. Jina hilo limetumika kwa muda mrefu kwenye nyanja ya siasa kumtambua kiongozi huyo wa upinzani.
Na mara nyingi limekuwa likitumiwa na vijana na hasa kwenye mitandao ya kijamii.
RAIS WA WANANCHI
Jina hili lilikuwa maarufu baada ya Raila Odinga kula kiapo chenye utata katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi kuwa rais wa wananchi.
Hayo yalijiri baada ya uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka wa 2017 kukumbwa na utata. Wakili aliyejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) Miguna Miguna ndiye aliyemuapisha.
MZEE WA VITENDAWILI
Raila alijipatia jina la "Mzee wa Vitendawili" kwa sababu ya kutumia vitendawili sana wakati wa kampeni za uchaguzi.
Ni jina ambalo lilitumika na wakosoaji wake wakati huo hasa Rais William Ruto kipindi akiwa Naibu Rais na mgombea uchaguzi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Source: BBC